Sport
Dollar
40,4343
0.24 %Euro
47,1614
0.49 %Gram Gold
4.349,9900
0.54 %Quarter Gold
0,0000
%Silver
0,0000
%Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilipongeza wasimamizi wa makubaliano hayo yaliyotiwa saini nchini Qatar siku ya Jumamosi.
Uturuki imekaribisha makubaliano yaliyotiwa saini kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na makundi ya waasi yenye lengo la kumaliza miongo kadhaa ya migogoro ya kivita mashariki mwa DRC.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na muungano wa makundi mbalimbali ya waasi, ikiwa ni pamoja na M23 (AFC/M23), walitia saini tamko la kanuni nchini Qatar siku ya Jumamosi kujitolea usitishaji vita wa kudumu na makubaliano ya kina ya amani yatakayotiwa saini katika muda wa mwezi mmoja, hatua ambayo inashangiliwa na wengi.
‘’Tunakaribisha Azimio la Kanuni lililotiwa saini kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na M23 chini ya uwezeshaji wa Qatar. Azimio hili ni hatua muhimu kuelekea suluhisho la amani na la kudumu la mzozo wa mashariki mwa DRC,’’ Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake Jumapili.
‘’Tunashukuru michango ya kiujenzi katika uimarishaji na maendeleo ya eneo la Maziwa Makuu na wahusika wote waliohusika katika mchakato huu, hususan Qatar, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika,’’ ilisema wizara hiyo.
Kukuza amani barani Afrika
‘’Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kukuza amani, usalama na utulivu barani Afrika,’’ iliongeza.
Hii ni ahadi ya kwanza ya moja kwa moja ya serikali ya DRC na waasi wa M23 tangu waasi hao kuteka miji miwili muhimu mashariki mwa Kongo katika hatua kubwa mapema mwaka huu.
Umoja wa Afrika pia ulipongeza mkataba huo mpya kama "maendeleo makubwa", ukisema: "Hii... inaashiria hatua kubwa katika juhudi zinazoendelea za kufikia amani ya kudumu, usalama, na utulivu mashariki mwa DRC na eneo kubwa la Maziwa Makuu".
Kundi la waasi la M23 ndilo kundi maarufu zaidi kati ya makundi yenye silaha yanayoendesha mashambulizi ya kutwaa udhibiti wa eneo la mashariki lenye utajiri wa madini la Congo.
Ghasia hizo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 8,000 wengi wao wakiwa ni raia tangu mwisho wa 2024, kwa mujibu wa serikali ya DRC, na kuongeza kuwa takriban milioni sita tayari wameuawa tangu mwaka 1996.
Huku watu milioni 7 wakiwa wamekimbia makazi yao nchini Kongo, Umoja wa Mataifa umeuita mzozo wa mashariki mwa Kongo "mojawapo ya majanga ya muda mrefu, magumu na makubwa ya kibinadamu Duniani."
Comments
No comments Yet
Comment