Tume huru iliyosikiliza ilibaini kuwa Manchester City haikutoa ushirikiano katika uchunguzi wa ligi kwenye baadhi ya tuhuma.
Manchester City imeingia kwenye kashfa kubwa baada ya kupatikana na hatia kwenye mashtaka 114 kati ya 115 ya kuvunja kanuni za kifedha za Ligi Kuu ya England.
Mashtaka hayo yanahusu kipindi cha 2009 hadi 2018, yakiangazia taarifa za fedha, malipo ya wachezaji na makocha, mikataba ya udhamini na masuala mengine ya kifedha. Tume huru iliyosikiliza kesi hiyo pia ilibaini kuwa City haikutoa ushirikiano katika uchunguzi wa ligi kwenye baadhi ya tuhuma.
Lakini hii stori ilianzia wapi? Mwaka 2018, jarida la Ujerumani la Der Spiegel liliweka wazi nyaraka za siri zilizovuja kupitia Football Leaks.
Nyaraka hizo zilihusishwa na Mreno Rui Pinto, ambaye alijulikana kama mtoa taarifa wa Football Leaks. Baadaye, taarifa hizo zikawa sehemu ya uchunguzi wa UEFA na Ligi Kuu.
City inamilikiwa kwa kiasi kikubwa na Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan, kutoka familia ilioko mamlakani Abu Dhabi.
City imekanusha makosa na sasa inaweza kukata rufaa. Adhabu inaweza kuwa faini, kupunguziwa pointi au hata kuondolewa EPL.
Wakati huo huo, kuna wanaotaka City ivuliwe mataji iliyoshinda katika kipindi hicho.
Wengine wanataka mataji hayo yapewe timu zilizomaliza nafasi ya pili. Lakini kwa sasa, hakuna uamuzi wa kupokonywa au kugawa mataji hayo.
Sasa macho yote yako kwenye rufaa na adhabu itakayoamuliwa.

