Eritrea imetangaza kukata mahusiano yote ya kidiplomasia na nchi jirani ya Ethiopia, baada ya Ethiopia kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea siku ya Alhamisi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Eritrea ilisema hatua ya kukata mahusiano imechukuliwa kwa kujibu hatua ya Ethiopia kuwafukuza wanadiplomasia hao kutoka Addis Ababa.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo ilisema Eritrea “haina chaguo jingine isipokuwa kujibu kwa hatua kama hiyo na kukata mahusiano yote ya kidiplomasia na Ethiopia, pamoja na madhara yote yanayoweza kutokana na hatua hiyo.”
Awali, Ethiopia ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea, ikidai kuwa walihusika katika shughuli ambazo zilikuwa “tishio la moja kwa moja” kwa usalama wa taifa wa Ethiopia.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Facebook, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ilisema imewatangaza wanadiplomasia hao 10 waliokuwa Addis Ababa kuwa watu wasiotakiwa —yaani watu wasioruhusiwa kuendelea kubaki nchini—kwa madai ya kujihusisha na shughuli zinazotishia moja kwa moja usalama wa taifa wa Ethiopia.
Wizara hiyo pia ilisema imeamua kuifunga Ubalozi wa Ethiopia mjini Asmara, mji mkuu wa Eritrea, ikitaja hatua hiyo kuwa ni majibu kwa kile ilichokiita “vitendo vya uhasama na uchochezi wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja” kutoka Eritrea kuelekea Ethiopia.
